‘Rafiki wa leo ni adui yako wa kesho’ ya Diamond na Ommy Dimpoz yanastaajabisha - DENIS KIBINDU

‘Rafiki wa leo ni adui yako wa kesho’ ya Diamond na Ommy Dimpoz yanastaajabisha

Japo hawakuzaliwa pamoja wala hawakuchangia damu, lakini machoni mwa watu walionekana ni kama mapacha kutokana na ukaribu wao wa kuambatana kama kumbi kumbi huku kila mmoja akimuita mzazi wa mwenzake baba au mama.
ommy-na-diampnd
Hakuna aliyetaka wala kusikia mwenzake akisemwa vibaya na watu wengine huku ukaribu huo ukipendwa na wengi japo wengine waliumizwa na ukaribu huo na kuwatupia matusi na maneno ya kejeli kwenye mitandao ya kijamii, lakini ilikuwa ni kama ‘sisimizi kumbeba tembo’ jambo ambalo lisingewezekana kirahisi.
Nimeamua kuanzia mbali ili niweze kukumbusha miaka miwili au mitatu iliyopita uvute taswira ya picha kwa kile unachokiona wakati Dully Sykes alipoachia wimbo wa ‘Utamu’ na kuamua kuwashirikisha wadogo zake Ommy Dimpoz na Diamond Platnumz kipindi ambacho ungeambiwa utaje wasanii watatu wanaofanya vizuri kwenye muziki usingeacha kuyataja majina ya wasanii hao wote wawili.
Nakumbuka miaka miwili iliyopita mwezi Juni, Dimpoz aliiambia Bongo5 kuwa kuna kolabo kati yake na Chibu inakuja na aliweza kusifia sana kwa kupamba huku akisema, “Watu kwanza najua wanasubiria kwa hamu sana lakini trust me nakuambia siku utakayosikia moto umewaka basi itakuwa ni balaa na unaelewa kwamba wamanyema kwanza hawakosei. Sijui itakuwaje, lakini ni balaa. Halafu projects zipo nyingi tu lakini watu wasubirie tu waone itakuwaje lakini nakuambia ukweli itakuwa hatari sana.”
10387972_1406589739623689_112378776_n
Siku zimepita na miaka imekwenda hakuna kolabo tuliyoiona lakini “ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni,” ndio tuliyoyaona. Ndipo nikaukumbuka wimbo malkia wa muziki wa Bongo Fleva, Lady Jaydee ‘Siku Hazigandi’ baada ya kuona urafiki uliogeuka undugu wa damu ukiteketea na kugeuka majivu baada ya kuunguzwa na mwanga wa tochi – ni kitu cha kushangaza na kisichowezekana lakini kwa hapo kiliwezekana.
Nilifurahi sana kuna busara iliyotumika kwa kila mmoja kukaa kimya bila ya kumshtumu mwenzake kwa lolote na kila mmoja akifanya kazi kivyake lakini ghafla nuru ya mwanga uliopo kugeuka giza baada ya usiku wa Jumanne hii mtandao wa Instagram ukigeuka uwanja wa ‘Kitchen Party’ kwa Ommy na Diamond kutupiana vijembe vya maneno ya kashfa na kuanza kutoleana siri ambazo kwa mashabiki hatuna uhakika nazo labda wao wenyewe wanajua juu ya ukweli wausemao kwa jamii.
Diamond alianza kwa kuandika kwenye kipande cha video ya wimbo mpya wa Rich Mavoko aliyoiweka kwenye mtandao huo, “Kushindana na Wasio Jua Raha sana hahahahahaha …….”
Ommy Dimpoz alijibu kwa kuandika:
Wazee Wa Kupanik Mbona Kama Povuuu Linawatoka #TeamMzikiMzuri VS #TeamUjanjaUjanja
#Kajiandae
#KabaliYao
#WeDontBuyViews
#MeNilijuaTunafanyaMzikiKumbeVitaaa
#NawajuaWazeeWaKuchambaNataniaTu
#PiaNawajuaKwaMitusiLakiniNishajiandaa
#NawaachiaUwanjaMweupeeeWalaSiblokuMtu
#NachangamshaBarazaKidogoooo
Diamond alishindwa kuvumilia naye aliandika, “Mtoto wa Kiume kumchukia Mwanaume Mwenzio kisa Kakataa kukupumulia nayo ni #KOKORO.”
Kwa watu wanaofahamu zaidi maneno ya mitaani wanaweza kufahamu kilichoandikwa ndani kina maana gani tena hayapaswi kuandikwa na wasanii wakubwa kama hawa kwenye hadhira hii. Wakati huo huo siku hizi mitandao ya kijamii inatembelewa mpaka na watoto wadogo, je watoto wao au hata ndugu zao wadogo wanaowalea na kuwategemea wakiona mtu anayemuheshimu nyumbani amefanya hivyo mitandaoni unafikiri itakuwaje?
Kumbukeni mlipotoka kwa kuwa ‘Adui yako wa leo ndio rafiki yako wa kesho, na rafiki yako wa leo ndio adui yako wa kesho’.

No comments

Powered by Blogger.